HOTUBA YA WAZIRI WA
MAENDELEO YA
JAMII, JINSIA NA WATOTO MHESHIMIWA SOPHIA M. SIMBA (MB.),
AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MATUMIZI
YA FEDHA KWA MWAKA 2014/15
A: UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba bunge lako tukufu baada ya
kuzingatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii,
sasa lijadili na kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Kawaida na ya
Maendeleo ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa mwaka 2014/15.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa
rehema kwa kutujalia kuwa na afya njema na hivyo kuweza kushiriki mkutano huu
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
3. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt.
Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter
Pinda, Waziri Mkuu na Mbunge wa Mpanda Mashariki kwa uongozi wao mahiri ambao
umewezesha kushamiri kwa usawa wa jinsia na uzingatiaji wa haki za mtoto katika
jamii ya watanzania. Mwenyezi Mungu awajalie afya njema ili waendelee
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
4. Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge, kwa uendeshaji bora wa
shughuli za Bunge. Tunaendelea kumuomba Mwenyezi Mungu awajalie afya njema ili
muweze kusimamia na kuratibu shughuli za Bunge kwa ufanisi.
5. Mheshimiwa
Spika, napenda kuchukua fursa hii kuishukuru Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ikiongozwa na Mwenyekiti wake mahiri Mheshimiwa
Saidi Mohamed Mtanda (Mb.) na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Kapteni Mstaafu John
Damiano Komba (Mb.) kwa kuichambua na kuijadili bajeti ya Wizara yangu. Ushauri
na maelekezo ya Kamati hiyo yametuwezesha kuboresha na kukamilisha bajeti
katika muda muafaka.
6. Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Samuel Sitta (Mb.) kwa
kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge
Maalum la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samiya Suluhu
Hassan (Mb.) kuwa Makamu Mwenyekiti. Aidha, nawapongeza Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa
Mbunge wa Kalenga na Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete kuwa Mbunge wa
Chalinze.
7. Mheshimiwa Spika, naomba nitangulize dua zangu kwa Mwenyezi Mungu azipokee
na kuzilaza mahali pema peponi roho za Marehemu William Agustino Mgimwa
aliyekuwa Mbunge wa Kalenga na marehemu
Said Bwanamdogo aliyekuwa Mbunge wa Chalinze. Bunge hili litawakumbuka
daima kwa michango yao.
8. Mheshimiwa
Spika, kwa masikitiko makubwa natumia fursa hii kuwapa pole wale
wote waliopatwa na majanga pamoja na kufiwa na ndugu, jamaa na wapendwa wao
katika matukio mbalimbali yaliyotokea nchini.
B: MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI
YA CCM YA MWAKA 2010 KWA KIPINDI CHA JANUARI, 2011 HADI MACHI, 2014
9. Mheshimiwa Spika, katika kipindi
cha mwaka 2013/2014, Wizara yangu
iliendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka
2010. Mafanikio ya utekelezaji wa Ilani kwa kipindi cha kuanzia Januari, 2011
hadi Machi, 2014 ni haya yafuatayo.
I. Ajira na Uwezeshaji wa Wananchi
10.
Mheshimiwa Spika, Ibara
ya 78 ya Ilani ya CCM, imeelekeza uimarishaji na upanuzi wa mafunzo ya Vyuo vya
Maendeleo ya Wananchi ili viweze kupokea vijana wengi zaidi na kuwapatia
mafunzo ya stadi na maarifa ya kisasa
katika fani za kilimo, biashara, ufundi na ujasiriamali.
11.
Mheshimiwa Spika, Mafunzo ya kuwapatia wananchi ujuzi na stadi
mbalimbali ili waweze kujiajiri na kuongeza uzalishaji mali na kipato ni muhimu
hasa katika kipindi hiki cha ukosefu mkubwa wa ajira. Wizara kupitia Vyuo 55
vya Maendeleo ya Wananchi, iliwapatia mafunzo
wananchi 146,383 wakiwemo wanawake 70,841 na wanaume 75,542
kupitia kozi fupi, kozi ndefu na mafunzo nje ya vyuo kwa kipindi cha Januari,
2011 hadi Machi, 2014. Mafunzo yanayotolewa ni pamoja na: uashi, useremala,
ufundi magari, ufundi chuma na uchomeleaji, kompyuta, ushonaji, umeme wa
majumbani, kilimo, ususi na upishi. Aidha, Wizara imeendelea kutoa mafunzo ya
ufundi stadi yanayoratibiwa na Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia vyuo 25
vya Maendeleo ya Wananchi ambapo kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaopata
mafunzo haya kutoka 1,125 mwaka 2013 hadi kufikia 2,722 mwaka 2014.
II. Kuyaendeleza Makundi Mbalimbali Watoto
12.
Mheshimiwa
Spika, Ilani ya CCM ya mwaka 2010 Ibara ya 204 (a), (h)
na (j) inaiagiza Serikali kukamilisha Sera ya Malezi na Makuzi ya Mtoto na
kupitisha Sera Fungamanishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto
ili watoto wote nchini waweze kunufaika kutokana na utekelezaji wake. Aidha,
Ibara hiyo inaitaka Serikali kutekeleza mikataba ya haki za mtoto iliyoridhiwa
na Bunge.
13.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza
azma hiyo, Wizara yangu imeendelea kufanya mapitio ya Sera ya Mtoto na
kutekeleza mikataba ya kimataifa kuhusu haki na maendeleo ya mtoto iliyoridhiwa
na Bunge lako tukufu. Wizara imefanya marekebisho ya Sera ya Maendeleo ya Mtoto
ya mwaka 2008 na imeandaa rasimu ya Sera ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya
Mtoto (2014) ili iweze kubeba masuala ya utoaji huduma fungamanishi na
shirikishi kwa mtoto. Masuala mengine yaliyoingizwa katika sera hiyo ni pamoja
na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu kwa watoto walio chini ya umri wa
miaka nane. Aidha, katika kuwezesha utekelezaji wa mikataba ya kimataifa
inayohusu haki na maendeleo ya mtoto, Wizara yangu inaandaa taarifa ya
utekelezaji wa mikataba hiyo ili kuiwasilisha katika vikao vya tatu, nne na
tano vya Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Mtoto (Convention on the Rights of the Child) katika mwaka 2014. Aidha,
Wizara yangu imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitatu (2013 –
2016).
Wanawake
14.
Mheshimiwa Spika, Ilani ya CCM
ya mwaka 2010 Ibara ya 205 (e) na (f) inaitaka Serikali kuimarisha mifuko
iliyopo ya mikopo na Benki ya Wanawake Tanzania ili wanawake wengi waweze
kufaidika kiuchumi.
15.
Mheshimiwa Spika, katika
kutekeleza azma hii ya Ilani, Wizara kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake
ilizipatia halmashauri 62 mikopo yenye jumla ya shilingi milioni 612 kwa ajili
ya kuwakopesha wanawake katika maeneo yao ili kuwaendeleza kiuchumi. Halmshauri zilipatiwa mikopo kupitia Mfuko
huu katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010/11 hadi 2013/14.
16.
Mheshimiwa Spika,
Serikali pia iliendelea kuiwezesha Benki ya Wanawake Tanzania ili kuwafikia
wananchi wengi zaidi hususan wanawake.
Katika kipindi cha Januari 2011 hadi Machi, 2014 Benki ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi
24,392,382,000 kwa wananchi 11,754, kati ya hao wanawake ni asilimia 88.
III. Elimu ya Juu
17. Mheshimiwa Spika, Ilani ya CCM ya mwaka 2010 Ibara ya 85 (e) imeelekeza Serikali kuongeza
udahili kwa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu. Wizara kupitia Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru iliendelea
kudahili wanafunzi katika ngazi ya shahada ya kwanza katika fani za Upangaji na
Usimamizi Shirikishi wa Miradi, Maendeleo ya Jamii, Maendeleo ya Jinsia na
Stashahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii. Jumla
ya wanachuo 546 wakiwemo wanawake 324 na wanaume 222 walidahiliwa kati ya
Septemba, 2011 hadi Septemba, 2013.
18. Mheshimiwa Spika, pamoja na kutoa mafunzo ya elimu ya juu, Wizara iliendelea kutoa mafunzo
ya taaluma ya maendeleo ya jamii kupitia vyuo vinane vinavyotoa mafunzo katika
ngazi ya Astashahada na Stashahada. Vyuo
hivyo ni Buhare, Missungwi, Rungemba, Uyole, Ruaha, Mlale, Mabughai na Monduli.
Jumla ya wanachuo 11,368 wakiwemo wanawake 7,463
na wanaume 3,905 walidahiliwa katika vyuo
hivi kwa kipindi cha Septemba, 2011 hadi Septemba, 2013. Kati ya idadi hiyo,
ngazi ya Stashahada ni 2,445 na
Astashahada ni wanachuo 8,923. Wahitimu katika fani hizi huajiriwa
katika ngazi ya halmashauri na huwezesha jamii kutekeleza majukumu yao ya
maendeleo kwa kutumia mbinu shirikishi na kuzingatia usawa wa kijinsia na haki
za mtoto hivyo kuifanya jamii kuwa na maendeleo endelevu.
IV. Demokrasia na Madaraka ya Umma
19.
Mheshimiwa Spika,
Ibara ya 188 (a) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, inaitaka Serikali
kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanajishughulisha na majukumu
yaliyoandikishwa kutekeleza na kwamba hayapati nafasi ya kujiendesha kinyume na
malengo yao. Kwa kuzingatia agizo hili la Ilani, Wizara yangu imekuwa ikichukua
hatua mbalimbali za kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Moja ya hatua hizo ni pamoja na kutoa elimu kwa
wadau 11,674 kati ya Januari, 2011 na Machi, 2014 kuhusu Sera ya Taifa ya
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Sheria ya NGOs Na.24 ya mwaka 2002
iliyorekebishwa mwaka 2005.
20.
Mheshimiwa Spika,
elimu hiyo ilitolewa kupitia Ofisi ya Msajili wa NGOs na mikutano ya wadau
iliyofanyika katika mikoa ya Morogoro, Mtwara, Njombe, Mwanza, Ruvuma, Lindi,
Mbeya na Tanga. Jumla ya Wadau 560 walipata elimu hii ikiwa ni pamoja na
Maafisa Maendeleo ya Jamii wa mikoa na wilaya 24, wawakilishi kutoka katika
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 536 na wananchi mbalimbali. Lengo la kufanya
hivyo ni kuziwezesha NGOs kufahamu wajibu wao na kujiendesha kwa mujibu wa
sheria na taratibu za nchi. Aidha, kwa upande wa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa
ngazi ya wilaya na mikoa elimu hiyo imelenga kuwajengea uwezo wa kufuatilia
shughuli za NGOs katika maeneo yao na kutoa taarifa kwa Wizara pindi
wanapobaini mashirika hayo kujiendesha kinyume na masharti ya usajili wao.
21.
Mheshimiwa Spika,
hatua nyingine ambazo Wizara yangu imechukua katika kutekeleza agizo hili la
Ilani ni pamoja na kuwateua Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwa wasajili wasaidizi
na waratibu wa mashirika haya katika ngazi za wilaya na mkoa ili kufuatilia
shughuli za mashirika hayo katika ngazi husika. Aidha, Wizara imekuwa
ikifuatilia na kutathmini utendaji na uendeshaji wa NGOs nchini ambapo kwa
kipindi cha Januari, 2011 na Machi, 2014, NGOs 55 zilitembelewa na kukaguliwa
katika maeneo yao ya utekelezaji. Aidha, taarifa za mwaka za fedha na kazi
zilizowasilishwa kutoka kwa mashirika 1,000 zilifanyiwa uchambuzi. Kutokana na
ufuatiliaji na tathmini ya shughuli za NGOs, shirika moja lilibainika
kujiendesha kinyume cha taratibu na kufutiwa usajili wake. Aidha, ilibainika
kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mengi yameendelea kutoa mchango mkubwa
katika huduma za kijamii na masuala ya kisera.
22.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka
2010, Wizara yangu ilikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na:
(i)
Uhaba wa wakufunzi wa kada mbalimbali
katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi;
(ii)
Upungufu wa vifaa vya kujifunzia na
kufundishia katika Vyuo tisa vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo 55 vya Maendeleo ya
Wananchi;
(iii)
Mahitaji ya mikopo ya Mfuko wa
Maendeleo wa Wanawake ni mengi ikilinganishwa na fedha zinazotolewa. Aidha,
mikopo inayotolewa kwa vikundi ni midogo isiyokidhi mahitaji halisi ya biashara
na mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa kwa wakopaji kutotosheleza kuwajengea
uwezo unaohitajika;
(iv)
Kutokuwepo kwa uwazi na uwajibikaji
kwa baadhi ya Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali.
C: HALI HALISI YA SEKTA YA MAENDELEO YA JAMII
NA CHANGAMOTO ZILIZOPO
23. Mheshimiwa Spika, Sekta ya maendeleo ya jamii hapa nchini imeendelea kukua na kutambulika na
wadau mbalimbali kutokana na mchango wake katika maendeleo ya taifa letu.
Naomba kuchukua fursa hii kueleza kwa kifupi hali halisi ya sekta hii katika
maeneo ya ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya kiuchumi, maendeleo ya
jinsia, maendeleo ya watoto na ushiriki wa mashirika yasiyo ya kiserikali
katika maendeleo nchini Tanzania.
Hali ya Ushiriki wa Wananchi katika Maendeleo
24.
Mheshimiwa Spika, maendeleo ya jamii kama dhana ni hatua mbalimbali
zinazowawezesha watu kutambua uwezo walio nao wa kubaini matatizo yao na
kutumia fursa na rasilimali zilizopo ili kuondokana na ujinga, maradhi, njaa na
umaskini kwa ujumla na hivyo kujiletea maisha bora. Msisitizo wa dhana hii ni
ushiriki wa watu katika kuamua, kupanga na kutekeleza mambo yote yanayohusiana
na maisha yao na nchi yao. Wataalamu
wa Maendeleo ya Jamii ni mhimili muhimu
kwa jamii katika kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kwani ndiyo wenye
jukumu la kushauri, kushawishi, kuelimisha, kuhamasisha na kuraghabisha wananchi kujiletea maendeleo kwa kutumia
mbinu shirikishi katika programu mbalimbali wanazoibua na kubuni. Hivyo,
wataalamu hao ni muhimu katika kuiwezesha jamii kuleta mabadiliko chanya kwa
kushiriki katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
25. Mheshimiwa Spika, Wataalamu wa
maendeleo ya jamii hufanya kazi katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na
wizara, wakala na mamlaka za Serikali,
Sekretariat za mikoa, halmashauri za miji, wilaya, manispaa na majiji, miji,
kata na vijiji. Wataalamu hao pia hufanya kazi na Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali na taasisi mbalimbali za sekta binafsi. Mfano, katika ngazi za
halmashauri takwimu zinaonesha kuwa kuna wataalamu wa maendeleo ya jamii 2,675
ambapo 1,381 hufanya kazi katika makao makuu ya halmashauri na 1,294 hufanya kazi katika Kata. Aidha, katika ngazi ya Sekretariat za mikoa kuna
jumla ya wataalamu 21. Wataalamu hawa hutoa
mchango mkubwa sana wa kuwaandaa wananchi kupokea na kutekeleza programu
mbalimbali za huduma kama za afya, elimu, maji, nishati na miradi mingine ya
kiuchumi na kijamii.
26. Mheshimiwa Spika, Sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka
1996 inasisitiza kuwepo kwa mtaalamu
mmoja kwa kila Kata hivyo mahitaji halisi ya wataalamu hao kwa ngazi husika ni
3,339. Kwa takwimu hizo upungufu wa wataalamu kwenye kata ni 2,045 sawa na
asilimia 61 ya mahitaji. Aidha, katika ngazi ya Sekretariati za mkoa upungufu
wa wataalamu hao ni asilimia 16. Hali hii inaathiri kwa kiasi kikubwa utekelezaji
wa shughuli za Sekta ya Maendeleo ya
Jamii. Katika kukabiliana na changamoto hii, Wizara yangu imeendelea
kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI kuhakikisha halmashauri zote zinaajiri wataalamu wa maendeleo ya jamii
katika ngazi ya Kata.
27. Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kutoa mafunzo na kuzalisha wataalamu wa Maendeleo ya
Jamii kupitia vyuo tisa vya maendeleo ya jamii nchini. Katika kipindi cha mwaka
2011/2012 hadi mwaka 2013/2014 jumla ya
wanachuo 11,914 walidahiliwa katika vyuo hivyo. Idadi hii kubwa ni matokeo ya
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na
kufundishia ikiwemo ujenzi na ukarabati wa majengo na miundombinu ya vyuo
hivyo.
28. Mheshimiwa Spika, wananchi wameendelea kunufaika na mafunzo yanayotolewa na Vyuo 55 vya
Maendeleo ya Wananchi vilivyo chini ya Wizara yangu. Idadi ya wananchi
wanaodailiwa katika vyuo hivyo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Mfano,
kati ya mwaka 2010/2011 na mwaka
2013/2014 idadi ya wananchi waliodahiliwa kwa mafunzo ya muda mrefu na muda
mfupi iliongezeka kutoka 32,133 hadi kufikia 40,692. Aidha, baadhi ya wananchi
walipata maarifa na ujuzi kupitia mafunzo nje ya chuo (outreach courses).
Mafunzo hayo yanawawezesha washiriki kujiajiri na kuajiriwa katika taasisi
mbalimbali. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa Vyuo hivi kwa miaka ya
hivi karibuni vimeanza kupokea vijana wengi waliohitimu mafunzo ya sekondari
sambamba na wale wa elimu ya msingi.
Hali ya Maendeleo
ya Jinsia
29. Mheshimiwa Spika, hali ya usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali hapa nchni imeendelea
kuimarika. Ukweli huu unadhihirishwa na ushahidi wa kitakwimu na taarifa
zilizopo katika maeneo ya ushiriki wa wanawake katika siasa na ngazi za
maamuzi; uwezeshaji wa wanawake kiuchumi; elimu, mafunzo na ajira; kuongezeka
kwa wanawake wajasiriamali (wadogo na wakati) na upatikanaji wa haki za
wanawake kisheria.
30. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
ushiriki wa wanawake katika ngazi za siasa na maamuzi, idadi ya mawaziri
wanawake imeongezeka kutoka asilimia 15 mwaka 2005 hadi asilimia 30 mwaka 2013,
wakuu wa mikoa wanawake kutoka asilimia 10 mwaka 2005 hadi asilimia 24 mwaka
2013. Majaji wanawake
pia wameongezeka kutoka asilimia 33 hadi
61 kwa kipindi hicho na
uwakilishi wa wanawake Bungeni umeongezeka kutoka asilimia 30.3 mwaka 2005 na
kufikia asilimia 36 ya wabunge wote mwaka 2013.
31. Mheshimiwa Spika, katika uwezeshaji wanawake kiuchumi taasisi za fedha na mifuko mbalimbali vimeendelea kutoa mikopo ya fedha
na mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake. Baadhi ya taasisi na mifuko hiyo ni
pamoja na Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake, Benki ya Wanawake Tanzania, Women
Convenant Bank, VICOBA na SACCOS. Mfano, Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake umetoa
mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 705 kwa kipindi cha kati ya mwaka
2011/12 na mwaka 2013/14.
32. Mheshimiwa Spika, Mila na desturi kandamizi bado ni changamoto katika kuhakikisha kuwa
kunakuwepo na usawa wa kijinsia kwa kuzingatia haki na usawa wa binadamu. Mila zinazoleta madhara kwa wanawake na hasa
watoto wa kike kama kukeketwa na kuozesha wasichana wa kike katika umri mdogo
zimeendelea na bado ni changamoto katika maeneo kadhaa ya nchi yetu. Wizara
inachukua hatua mbalimbali kupambana na changamoto hizi ambazo ni pamoja na
kutoa elimu kwa kushirikiana na wadau hasa NGOs na washirika wa maendeleo na
kuiwezesha Kamati ya Kitaifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake ili iweze
kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Hali ya Maendeleo ya Watoto
33.
Mheshimiwa Spika, Watoto ni sehemu muhimu ya jamii na ndiyo tegemeo ya
Taifa lolote. Watoto wanahitaji kukua na
kuwa raia wema, hivyo wanatakiwa kupewa haki na mahitaji yao ya msingi ikiwa ni
pamoja na: kuishi, kupewa malezi stahiki, kulindwa, kuendelezwa kiakili kwa
kutambua na kukuza vipaji vyao, kutobaguliwa na kushirikishwa.
34. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Taifa ya Idadi ya Watu na Makazi ya
mwaka 2012, idadi ya watoto chini ya miaka 18 Tanzania Bara ni 21,866,258 sawa
na asilimia 50.1 ya idadi ya watu wote.
Kati yao wasichana ni 10,943,846 na wavulana ni 10,922,412.
35. Mheshimiwa Spika, Pamoja na Serikali kuweka mazingira wezeshi ya kuwapatia watoto haki zao
kupitia sera,sheria, mipango, programu na mikakati mbalimbali, bado maendeleo
ya mtoto yanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Changamoto hizo ni pamoja na: ukatili dhidi ya watoto, kuwepo kwa watoto
wanaoishi katika mazingira hatarishi, kushuka kwa maadili, ndoa na mimba za
utotoni.
36. Mheshimiwa Spika, Kumekuwepo na jitihada mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo ikiwa
ni pamoja na uanzishwaji wa Kituo cha Huduma za Pamoja (One Stop Centre) kwa majaribio
katika Hospitali ya Amana - Manispaa ya Ilala kwa ajili ya kuhudumia watoto
mbalimbali wanaofanyiwa aina mbalimbali za ukatili na kutoa elimu kwa wazazi na
walezi juu ya wajibu wao katika malezi ya watoto. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na wadau imewezesha
kuanzishwa kwa mtandao wa mawasiliano wa kusaidia watoto (Child Helpline) namba 116 kwa ajili
ya jamii inayotumika kutoa taarifa za ukatili dhidi ya watoto na ukiukwaji wa
haki za watoto. Namba hii imeanza kufanya kazi katika maeneo machache kwa
majaribio na utekelezaji wa kazi zake unaonesha mafanikio mazuri hadi sasa.
Hali ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
37.
Mheshimiwa
Spika, idadi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali chini ya
Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002 iliyorekebishwa mwaka 2005 imeendelea kukua
mwaka hadi mwaka. Kufikia tarehe 17
Machi, 2014 idadi ya mashirika hayo ilifikia 6,427 kutoka mashirika 3,000
yaliyokadiriwa kuwepo mwaka 2001 wakati Sera ya Taifa ya NGOs ilipokuwa
inaandaliwa. Hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100. Kati ya mashirika
yaliyosajiliwa, 254 ni ya kimataifa na 6,173 ni ya ndani ya nchi yanayofanya
kazi katika ngazi za wilaya, mkoa na taifa.
38.
Mheshimiwa
Spika, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yameendelea
kutambulika kama wadau na wabia muhimu katika maendeleo. Mashirika haya
yanajishughulisha na kazi mbalimbali ikiwemo elimu, mazingira na mabadiliko ya
tabianchi, afya, maendeleo shirikishi, haki za binadamu, maendeleo ya jinsia,
ushawishi na utetezi, kinga ya jamii, haki za watoto, kilimo, maji na ustawi wa
jamii.
39.
Mheshimiwa
Spika, kuongezeka kwa idadi na shughuli za NGOs katika
nchi yetu ni matokeo ya mazingira wezeshi yanayoendelea kuboreka mwaka hadi
mwaka. Hii ni pamoja na uwepo wa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali ya mwaka 2001, Sheria ya NGOs Na.24 ya mwaka 2002 iliyorekebishwa
mwaka 2005 na Kanuni za Maadili za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali za mwaka
2008. Aidha, muundo wa kitaasisi unaowezesha NGOs kujitawala kwa uhuru na
kujiratibu umeendelea kuwepo ikiwemo:
Bodi ya Uratibu wa NGOs, Baraza la Taifa la NGOs, Maafisa Maendeleo ya
Jamii wa Wilaya na mikoa ambao ni Wasajili Wasaidizi na mitandao ya NGOs ya
wilaya, mkoa na taifa.
40.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na kuimarika kwa hali ya Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali hapa nchini, bado kuna changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi.
Changamoto zilizopo ni pamoja na sehemu kubwa ya shughuli za Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali kutegemea wafadhili kutoka nje na kutokuwa na vyanzo vya uhakika
vya ndani ya nchi hivyo kuathiri uendelevu wa shughuli hizo pindi wafadhili hao
wanapositisha misaada. Changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa Kamati za Maadili
ya NGOs katika baadhi ya mikoa na wilaya kunakoathiri uwezo wa NGOs kujitawala
katika kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali na
uendeshaji wa mashirika hayo.
41.
Mheshimiwa
Spika, katika kutatua changamoto hizo wizara yangu
imechukua hatua mbalimbali. Mojawapo ya hatua hizo ni kuhimiza Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali kutumia fursa ya marekebisho ya Sheria ya NGOs yaliyofanyika
mwaka 2005 kuanzisha na kuendeleza miradi ya kuzalisha faida kwa ajili ya
kutekeleza malengo yao hata pale wafadhili wanapositisha misaada. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Baraza la
Taifa la NGOs inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuliwezesha kuanzisha
Kamati za Maadili ya NGOs katika ngazi ya wilaya na mikoa ikiwa ni utekelezaji
wa Kanuni za Maadili ya NGOs.
Mafanikio
42.
Mheshimiwa
Spika, mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa
bajeti ya mwaka 2013/2014, ni pamoja na:
(i)
Idadi ya
vituo vya kutolea mikopo kwa wajasiriamali wadogo hususan wanawake
imeongezeka toka vituo 21 mwaka 2012/13 hadi vituo 50 mwaka 2013/14, sawa na ongezeko la
asilimia 58;
(ii)
Matawi ya
Benki ya Wanawake Tanzania yameongezeka toka tawi moja mwaka 2009/10 hadi
matawi mawili mwaka 2013/14;
(iii)
Kuongezeka
kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyosajiliwa toka mashirika 3,000 mwaka
2001/02 hadi mashirika 6,427 mwaka
2013/14;
(iv)
Wanafunzi
waliojiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika Vyuo 25 vya Maendeleo ya Wananchi
wameongezeka toka wanafunzi 1,125 mwaka 2013 hadi wanafunzi 2,722 mwaka 2014;
(v)
Wanafunzi
waliojiunga na mafunzo ya elimu ya wananchi (Kozi ndefu) katika Vyuo 55 vya
Maendeleo ya Wananchi wameongezeka toka wanafunzi 6,586 mwaka 2013 hadi
wanafunzi 7,144 mwaka 2014;
(vi)
Kuongezeka
kwa Halmashauri zilizopata mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake toka
Halmashauri 19 mwaka 2008/09 hadi Halmashauri 38 mwaka 2013/14; na
(vii)
Kuongezeka
kwa Madawati ya Jinsia na Watoto toka madawati 9 mwaka 2008 hadi madawati 417
mwaka 2014.
43.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Sekta ya
Maendeleo ya Jamii inakabiliwa na changamoto zifuatazo:
(i)
Uhaba wa
wakufunzi wa kada mbalimbali katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya
Wananchi;
(ii)
Ukosefu wa
vyombo vya usafiri katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Vyuo vya Maendeleo ya
Jamii na uchakavu wa vyombo vya usafiri Makao Makuu ya Wizara;
(iii)
Upungufu wa
vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika Vyuo tisa vya Maendeleo ya Jamii na
Vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi;
(iv)
Uchakavu wa
majengo na miundombinu katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Maendeleo
ya Wananchi;
(v)
Kuendelea
kukua kwa madeni ya watumishi, wakandarasi na watoa huduma mbalimbali Wizarani.
Madeni yamefikia shilingi 2,558,735,065 katika deni hilo shilingi
774,308,379.84 ni madeni ya watumishi, shilingi 773,166,431.80 ni madeni ya
wazabuni na shilingi 1,011,260,253.36 ni madeni ya wakandarasi;
(vi)
Fedha
kutolewa na Wizara ya Fedha bila kuzingatia Mpango Kazi na Mtiririko wa
Mahitaji ya Fedha;
(vii)
Mahitaji ya
mikopo ya Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake ni mengi ikilinganishwa na fedha
zinazotolewa. Aidha, mikopo inayotolewa kwa vikundi kuwa kidogo isiyokidhi
mahitaji halisi ya biashara na mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa kwa
wakopaji kutotosheleza kuwajengea uwezo unaohitajika;
(viii)
Kupanua
huduma za Benki ya Wanawake Tanzania ili kuwafikia wanawake wengi zaidi; na
(ix)
Kutokuwepo
kwa uwazi na uwajibikaji kwa baadhi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
(x)
Kuongezeka
kwa matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii.
D: MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA
2013/14 NA MALENGO YA MWAKA 2014/15
44.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara yangu iliendelea kusimamia utekelezaji wa
majukumu yake kulingana na malengo yaliyopangwa. Katika bajeti ya mwaka
2013/14, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto iliidhinishiwa jumla ya
shilingi 25,964,170,000 kwa ajili ya matumizi ya Kawaida na Maendeleo. Kati ya
fedha za matumizi ya kawaida, shilingi 5,397,496,000 ni kwa ajili ya matumizi
mengineyo na shilingi 8,656,002,000 kwa ajili ya malipo ya mishahara na
shilingi 11,910,672,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
45.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 15 Mei, 2014, Wizara ilikuwa imetumia jumla ya
shilingi 10,305,162,100 sawa na asilimia 100 ya fedha za Matumizi ya Kawaida
zilizopokelewa na shilingi 2,923,620,590 sawa na asilimia 100 ya fedha za
Maendeleo zilizotolewa.
46.
Mheshimiwa
Spika, naomba kuwasilisha utekelezaji wa mpango wa mwaka 2013/14 na malengo ya mwaka 2014/15 kwa
kuzingatia maeneo yafuatayo:
Maendeleo ya Jamii
47.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2013/2014 Wizara yangu ilidahili
na kutoa mafunzo kwa wanachuo 2,869 kupitia vyuo tisa vya Maendeleo ya Jamii
vya Tengeru, Buhare, Rungemba, Monduli, Missungwi, Ruaha, Uyole, Mlale na
Mabughai. Wanachuo 2,036 walidailiwa katika ngazi ya cheti, 591 katika ngazi ya
stashahada, 234 ngazi ya shahada na 8 katika ngazi ya Stashahada ya Uzamili. Aidha, Wizara yangu ilikarabati majengo na
miundombinu katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale, Misungwi na Mabughai.
Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kukamilisha jengo la maktaba ya
Chuo cha Tengeru na maabara ya kompyuta katika chuo cha Mabughai kwa lengo la
kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
48. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2013/14 Wizara
yangu ililipa shilingi 84,114,523 zikiwa ni gharama za ujenzi zilizoongezeka
katika ujenzi wa bwalo, jiko na nyumba za watumishi katika vyuo vya Maendeleo
ya Wananchi vya Mputa na Muhukuru mkoani Ruvuma. Aidha, Wizara ilifanya ukarabati wa mabweni
na jengo la utawala katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tarime; ukarabati wa
nyumba za watumishi na uwekaji wa mfumo wa umeme katika chuo cha Maendeleo ya
Wananchi Mwanhala; ukarabati wa jengo la utawala na bweni katika chuo cha
Maendeleo ya Wananchi Kilwa Masoko; ukarabati wa mabweni na nyumba za watumishi
katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msaginya, Mputa, Sofi na Singida; ujenzi
wa vyoo katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Masasi na Chilala; na kuvipatia
vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 25 vifaa vya kujifunzia na kufundishia masomo ya
ufundi stadi.
49. Katika mwaka 2014/2015 Wizara yangu itaendelea
kudahili na kutoa mafunzo kwa wananchi na pia itakarabati majengo na
miundombinu ya vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vya Mto wa Mbu, Msaginya na
Nandembo.
50. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha mafunzo ya maendeleo ya
wananchi kwa kutoa huduma kwa watoto kupitia vituo vya kulelea watoto ndani ya
vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 55 ambapo jumla ya watoto 1,033 walinufaika. Kuwepo kwa vituo hivi katika vyuo vya Maendeleo ya
Wananchi kumewawezesha watumishi katika vyuo hivi na jamii inayovizunguka vyuo
hususan wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali kwa
uhuru zaidi. Aidha, vituo hivi vimewawezesha washiriki wanawake 97 wenye watoto
wadogo kupata mafunzo wakiwa na watoto wao vyuoni.
51. Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha
mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuimarisha vituo vya kulelea watoto katika
vyuo 55 vya maendeleo ya wananchi kwa kutoa vifaa vya kufundishia na kujifunzia
na kutengeneza viwanja vya michezo. Aidha, Wizara itawajengea uwezo wakufunzi
30 kwa ajili ya kuwawezesha kupata elimu ya kuendesha vituo vya kulelea watoto
wadogo ikiwa ni pamoja na kuwapatia ujuzi wa kufundisha watoto hao elimu ya awali.
Mafunzo ya kuwajengea uwezo wakufunzi katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi
yatakuwa yanatolewa kwa awamu kulingana na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya
Elimu.
Maendeleo ya Jinsia
52. Mheshimiwa Spika, uwezeshaji wanawake kiuchumi
ni suala muhimu katika kufikia usawa wa kijinsia na kupunguza umaskini wa
kipato katika jamii. Katika mwaka 2013/14, Wizara kupitia Mfuko wa Maendeleo wa
Wanawake iliziwezesha Halmashauri 39 kutoa mikopo yenye thamani ya shillingi
milioni 428. Katika kuhakikisha Mfuko unafikia malengo yaliyopangwa, Wizara
ilifuatilia utendaji wa Mfuko katika mikoa tisa na kuiwezesha Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kufuatilia utekelezaji wa Mfuko katika
Halmashauri mbalimbali. Halmashauri ambazo Kamati ya Bunge ilifanya ufuatiliaji
huo ni Kinondoni, Ilala, Kibaha, Korogwe na Jiji la Tanga. Mikoa ambayo Wizara
ilifuatilia shughuli za Mfuko ni Arusha, Manyara, Singida, Pwani, Tanga,
Katavi, Rukwa, Morogoro na Kagera. Matokeo ya ufuatiliaji yanaonesha kwamba
Halmashauri nyingi hazichangii asilimia tano ya mapato yao kama inavyotakiwa.
Kutokana na matokeo hayo, Halmashauri ziliagizwa kuchangia katika Mfuko huo.
53. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu
itaendelea kutoa fedha kwa Halmashauri nyingine zitakazokuwa zimemaliza
marejesho pamoja na kufanya ufuatiliaji kwa mikoa na halmashauri zilizobaki.
Napenda kutumia fursa hii kuzikumbusha halmashauri zote zilizokopeshwa
kuzingatia mkataba wa marejesho. Aidha, nazikumbusha halmashauri zote
nchini kuchangia asilimia tano ya mapato
yao kwenye Mfuko wa Maendeleo wa wanawake ili wanawake wengi zaidi wanufaike na
huduma za Mfuko huu.
54. Mheshimiwa
Spika, kupitia Benki ya Wanawake
Tanzania huduma za kibenki zimewafikia
wananchi wengi zaidi wakiwepo wanawake kwani imeweza kufungua tawi la pili la Benki ya Wanawake Tanzania eneo la
Kariakoo Mkoa wa Dar es Salaam, Mtaa wa
Agrey/Likoma. Aidha, vituo 29 vya
kutolea mikopo na mafunzo kwa wajasiriamali vimefunguliwa katika Mikoa ya Dar
es Salaam, Dodoma na Mwanza. Vituo hivyo ni
kama ifuatavyo: Dar es Salaam (Tabata Kisukuru, Mbande, Sabasaba, Ubungo
Kibangu, Chanika, Chamazi na Kunduchi Mtongani); Dodoma (Airport, Chamwino,
Ipagala, Posta, Hazina Kikuyu, Kizota, Savanna Kikuyu, Chang’ombe, Mnadani, Veyula, Mpwapwa, Kongwa
na Mbande); na Mwanza (Nyakato, Igogo, Nyegezi, Pansiansi, Igoma, Kisesa, Magu,
Misungwi na Kitangiri). Kwa mwaka 2014/15, Wizara yangu itaendelea kutoa ruzuku
kwa Benki ya Wanawake Tanzania ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.
55. Mheshimiwa Spika, Ukatili wa kijinsia
umeendelea kuwa ni tatizo katika jamii zetu ambapo wananchi wengi wameendelea
kuumizwa na kuteseka na hata kuuawa kutokana na vitendo vya kikatili
vinavyofanyika hapa nchini. Mwaka
2013/2014, Wizara ilifanya tathmini ya mafunzo yaliyotolewa kwa Kamati za
Ulinzi na usalama katika Mkoa wa Manyara kuhusiana na kupiga vita ukatili wa
kijinsia. Moja ya matokeo ya tathmini hiyo imeonyesha kuwa Kamati husika
zinahitaji kujengewa uwezo zaidi ili ziweze kufanya kazi zake kikamilifu.
Katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kufanya tathmini ya mafunzo
yaliyotolewa kwa Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya kuhusu mbinu za
kutokomeza ukatili katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Mara. Aidha, itaendelea
kuzijengea uwezo kamati za ulinzi na usalama
ili ziweze kupambana na kutokomeza ukatili katika ngazi ya wilaya na
kuendelea kuiwezesha Kamati ya Kitaifa
ya Kuzuia na Kuondoa Ukatili Dhidi ya
Wanawake na Watoto ili iweze
kutekeleza shughuli zake kikamilifu.
56. Mheshimiwa Spika, suala la uingizaji wa masuala
ya kijinsia katika sera, mipango na bajeti limekuwa likitiliwa mkazo ili
kuhakikisha kuwa mipango na bajeti za kila sekta, idara na taasisi mbalimbali
inawanufaisha wote, yaani wanawake, wanaume, wavulana na wasichana. Katika
kipindi cha mwaka 2013/14, Wizara kupitia wataalamu wake ilifanya tathmini ya
uingizaji wa masuala ya jinsia katika Halmashauri 6 ambazo ni Halmashauri ya
Jiji la Tanga na Arusha, Halmashauri za Wilaya ya Iringa na Moshi pamoja na
Manispaa ya Temeke na Morogoro. Lengo la
tathmini ilikuwa ni kubaini mafanikio na changamoto zinazojitokeza katika
uingizaji wa masuala ya jinsia katika sera na mipango na bajeti mbalimbali. Katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kutoa
mafunzo ya uingizaji wa masuala ya jinsia kwa wataalamu mbalimbali ili waweze
kuelewa na kutekeleza mkakati huu ikiwa ni pamoja na kukamilisha Sera ya Taifa
ya Jinsia. Aidha, Wizara imeanza mchakato wa kuandaa taarifa ya hali ya jinsia
nchini (Tanzania Country Gender Profile) na kuanzisha benki ya Takwimu ya usawa
wa jinsia. Taarifa hii na Benki ya Takwimu zitawezesha kufanya maamuzi,
upangaji wa mipango, ushawishi na uhamasishaji kuhusu masuala ya jinsia ili
kuwa na maendeleo endelevu. Aidha,
zitasaidia kupima utekelezaji wa mipango na programu mbalimbali kuona kama
zinaweza kupunguza changamoto za kijinsia na kuleta usawa unaotarajiwa.
57. Mheshimiwa Spika, mwaka 2013/2014, Wizara iliandaa rasimu ya 7 na 8 ya nchi ya Mkataba wa
Kuondoa Aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake. Maandalizi ya taarifa hiyo
yaliwashirikisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Watendaji wa Madawati ya
Jinsia kutoka Wizara mbalimbali, asasi za kijamii na Maafisa wa Maendeleo
Jamii. Rasimu ya Taarifa hiyo imekamilika na inatarajiwa kujadiliwa na wadau
mbalimbali wakiwemo Kamati ya Bunge ya Sekta ya Maendeleo ya Jamii kwa lengo la
kupata maoni zaidi kwa ajili ya kuiboresha.
58. Mheshimiwa Spika, tarehe 8 Machi kila mwaka,
Wizara imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kuratibu maadhimisho ya Siku
ya Wanawake Duniani. Kwa mwaka 2013/2014, maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani yalifanyika kimkoa ambapo lengo kuu lilikuwa ni kuwakutanisha wanawake
wa ngazi zote ili waweze kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali
yanayowakabili, kubaini fursa zilizopo katika kujiletea maendeleo na kutafuta
ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili. Katika mwaka 2013/14, Wizara yangu iliratibu
maadhimisho ya siku hiyo katika ngazi ya mikoa ambapo Kauli mbiu ilikuwa ni “Chochea Mabadiliko Kuleta Usawa wa
Kijinsia” Kauli mbiu hii inasisitiza na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa
kuzingatia masuala ya jinsia katika kupanga na kutekeleza mikakati na mipango
ya maendeleo kwa kuzingatia ushiriki stahiki wa wanawake, wanaume, wavulana na
wasichana katika kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla. Kwa mwaka
2014/15, Wizara itaratibu maadhimisho haya Kitaifa ili kuweza kupima mafanikio
yaliyopatikana katika miaka mitano (2010 – 2015) katika juhudi za kumwendeleza
mwanamke pamoja na kubainisha changamoto zilizojitokeza kwa kipindi hicho toka
maadhimisho haya yalipofanyika kitaifa mwaka 2010.
59. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza mikataba na
maazimio mbalimbali ambayo nchi imesaini na kuridhia, mwaka 2013/14, Wizara
ilishiriki katika mkutano wa 58 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake na mkutano wa
nchi za Maziwa Makuu kuhusu masuala ya jinsia. Lengo la mikutano hiyo ni
kutafuta mbinu za pamoja za kukabiliana na changamoto mbalimbali, kubadilishana
uzoefu na kukubaliana maeneo muhimu ya utekelezaji katika kuleta usawa wa
kijinsia na maendeleo ya wanawake katika nchi husika. Katika mwaka 2014/15,
Wizara itaendelea kushiriki na kutoa mchango wake katika mikutano ya kikanda na
kimataifa kuhusu utekelezaji wa masuala ya usawa wa kijinsia na kuwaendeleza
wanawake.
Maendeleo ya Watoto
60.
Mheshimiwa
Spika, maendeleo ya taifa lolote duniani hutegemea sana
namna ambavyo linawalinda na kuwakuza watoto wake. Kwa kuzingatia hilo, Wizara
yangu imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto
zinazowakabili watoto hapa nchini.
61.
Mheshimiwa
Spika, mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliandaa mpango kazi
wa jamii wa kudhibiti tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani. Lengo
likiwa ni kuongeza ushiriki wa wadau katika kudhibiti na kuondoa tatizo hilo
kwa kuwaelimisha na kuhamasisha ili wabebe jukumu la kuwapatia watoto mahitaji
na haki zao za msingi. Utekelezaji wa Mpango kazi unahusisha familia, jamii,
serikali, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wabia wa maendeleo. Katika
mwaka 2014/2015, Wizara itasambaza mpango katika mikoa yote na kuratibu utekelezaji
wake.
62.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imefanya
marekebisho ya Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 kuwa Sera ya Malezi,
Makuzi na Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2014 ili iweze kujumuisha masuala ya
utoaji huduma fungamanishi na shirikishi za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya
Mtoto. Aidha, Sera hiyo imezingatia masuala ya kukabiliana na changamoto
zinazotokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na upatikanaji wa
huduma za malezi na makuzi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka nane. Katika
mwaka 2014/2015, Wizara itakamilisha Sera hiyo na mkakati wake wa utekelezaji.
Aidha, Wizara itasambaza kwa wadau sera na mkakati huo kwa ajili ya
utekelezaji.
63.
Mheshimiwa
Spika, ukatili dhidi ya watoto ni moja ya changamoto zinazoathiri
malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto. Katika kupunguza matukio ya ukatili huo,
mwaka 2013/2014 Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iliandaa
Mpango Kazi Shirikishi wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Watoto wa mwaka 2013 hadi
2016. Aidha, Wizara yangu iliwezesha
kufanyika kwa mkutano wa mwaka wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuzuia Ukatili
dhidi ya Mtoto ambapo sekta zote zinazohusiana na maendeleo ya mtoto zilitoa
taarifa kuhusu mapendekezo ya namna ya kutekeleza mpango huo. Pia, Wizara
iliandaa mkutano uliowakutanisha watekelezaji wa Mpangokazi wa miaka mitatu wa
kuzuia ukatili wa watoto na wadau wa maendeleo na tayari wadau kadhaa wa
maendeleo wajitokeza na kuanza kuchangia fedha za utekelezaji wa baadhi ya kazi
zilizoainishwa katika mpango huu. Tunawashukuru sana wadau hawa. Katika mwaka
2014/2015, Wizara itaendelea kuratibu na kusimamia mpango huo kwa kushirikiana
na kikosi kazi hicho.
64.
Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu pia iliandaa kitini cha elimu ya
malezi kwa familia kuhusu kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto. Kitini hicho
kitatumiwa na wawezeshaji jamii katika kuwajengea uwezo wazazi na walezi ili
kudhibiti ukatili dhidi ya watoto.
Aidha, kuanzia ngazi ngazi ya familia Wizara ilitoa mafunzo kuhusu
Kitini hicho kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka halmashauri za Hai, Temeke,
Magu na Kasulu. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuratibu usambazaji
wa kitini hicho katika halmashauri nyingine.
65.
Mheshimiwa
Spika, vilevile, Wizara iliendelea kuratibu utoaji wa
taarifa za ukatili dhidi ya watoto kupitia namba ya simu 116 inayosimamiwa na
Shirika Lisilo la Kiserikali la C-SEMA. Hadi kufikia Machi, 2014 jumla ya simu
6,188 zilipigwa kupitia namba hiyo na kufanyiwa kazi. Mwaka 2014/15, Wizara
itaendelea kuratibu na kusimamia mtandao huo na kuendelea kutathmini ili
kuwezesha kupeleka huduma hii katika maeneo mengine ya nchi.
66.
Mheshimiwa
Spika, Watoto wanayo haki ya msingi ya kushiriki na
kushirikishwa katika masuala yote yanayowahusu. Katika kuhakikisha ushiriki wa
watoto katika kutoa maoni yao, mwaka 2013/2014, wizara iliandaa Mkutano Mkuu wa
Baraza la Watoto ili kupitia rasimu ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Aidha, wizara yangu iliratibu utekelezaji wa shughuli za mabaraza
ya watoto katika ngazi ya Wilaya/Mikoa pamoja na Azimio la Bujumbura kuhusu
haki na ustawi wa watoto. Katika mwaka
2014/2015, Wizara itaendelea kushirikiana na Halmashauri kuimarisha Baraza la
Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mabaraza ya watoto ya mikoa
na wilaya ili yaweze kutoa fursa nzuri za ushiriki wa watoto katika maeneo
husika.
67.
Mheshimiwa
Spika, Katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliratibu
maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo yaliadhimishwa katika ngazi ya
mkoa. Katika maadhimisho hayo, kila mkoa ulipata fursa ya kuadhimisha siku hii
muhimu kulingana na mazingira na uhitaji wa mkoa husika. Kauli mbiu ya mwaka 2013/2014 ilikuwa ni “Kuondoa Mila zenye kuleta Madhara kwa
Watoto: ni Jukumu Letu Sote”. Lengo la kaulimbiu hiyo ni kuhamasisha jamii
kubaini baadhi ya mila ambazo zimekuwa zikileta madhara kwa watoto na kuweka mikakati ya kuzitokomeza.
68.
Mheshimiwa
Spika, Vile vile, Wizara yangu iliratibu maadhimisho ya
siku ya Familia Duniani ambayo
yalifanyika kimkoa. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ilikuwa ni “Imarisha na Endeleza Ushirikiano na
Mshikamano wa Familia na Makundi Mbalimbali ya Jamii”. Kauli mbiu hii inasisitiza wazazi, walezi na
jamii kuwajibika kwa pamoja katika malezi ya familia. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea
kuratibu maadhimisho ya siku hizo kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu haki na
ustawi wa mtoto na maendeleo ya familia.
Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
69.
Mheshimiwa
Spika, Katika kipindi cha mwaka 2013/2014, Serikali
iliendelea kusajili Mashirika Yasiyo ya Kiserikali chini ya Sheria ya NGOs
Na.24 ya mwaka 2002. Jumla ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 435 yalipatiwa
usajili katika ngazi ya wilaya, mkoa, taifa na kimataifa. Kati ya hayo, mashirika
ya kimataifa ni 23 na mashirika ya ndani ya nchi yaani ya ngazi za wilaya, mkoa
na taifa ni 412. Hii imefanya idadi ya
NGOs kuongezeka kutoka mashirika 5,992 mwezi Julai, 2013 na kufikia mashirika
6,427 mwezi Machi, 2014 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2014/15,
Wizara yangu itaendelea na usajili wa mashirika hayo.
70.
Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu pia iliratibu shughuli za NGOs kwa
kuwezesha ushiriki wa wadau katika utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali. Hii ni pamoja na kuiwezesha Bodi ya uratibu wa NGOs
kukagua shughuli za NGOs 21 na kufanya vikao vitatu katika mikoa ya Tanga,
Lindi na Mbeya. Vikao hivyo vilifikia maamuzi mbalimbali ikiwemo utatuzi wa
migogoro katika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Aidha, Wizara kupitia Bodi ya
Uratibu wa NGOs ilikutana na wadau 175 na kujadili mafanikio na changamoto
zinazozikabili NGOs katika mikoa husika na kutoa elimu kuhusa Sera ya Taifa ya
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 na Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka
2002. Wizara pia imeanzisha utaratibu wa
kukutana na NGOs zinazofanyakazi za watoto na wanawake na mapendekezo ya
kuboresha ushirikiano yameandaliwa. Kwa
mwaka 2014/15, Wizara yangu itaendelea kuiwezesha Bodi ya Uratibu wa NGOs
kufanya vikao vinne na kukutana na wadau ili kuboresha uratibu wa NGOs nchini
na pia itaendelea na utaratibu wa kukutana na NGOs zinazofanyakazi na watoto na
wanawake ili kuboresha ushirikiano na utekelezaji wa majukumu haya.
71.
Mheshimiwa
Spika, katika kuendelea kujenga mazingira wezeshi na
kuboresha uratibu wa mashirika haya, Wizara yangu itatekeleza mambo mbalimbali
katika kipindi cha mwaka 2014/2015. Kazi hizo ni pamoja na kufuatilia na
kutathmini mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na hali ya uendeshaji wa
mashirika hayo hapa nchini.Aidha, itawezesha kufanyika kwa tathmini kuhusu
ufanisi wa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kujenga
mazingira wezeshi kwa NGOs. Vilevile, Serikali kupitia Wizara yangu itawezesha
kufanyika kwa mafunzo ya ndani kuhusu usajili, ufuatiliaji na tathmini ya
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya na
mikoa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji ili kuboresha utoaji wa
huduma za usajili na uratibu katika ngazi
husika.
Uratibu wa Sera na Mipango
72.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
2013/14 uratibu na mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 pamoja
na mkakati wake ulifanyika. Katika mwaka 2014/15, uratibu wa mapitio ya Sera ya
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 na tathmini ya utekelezaji wa Sera
ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 na Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo Ya
Kiserikali ya mwaka 2001utafanyika. Aidha, uratibu wa mipango na bajeti ya
mwaka 2015/16 pamoja na uandaaji wa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa Wizara
utaandaliwa ili kuimarisha ukusanyaji, uhifadhi na usimamizi wa takwimu na
taarifa za sekta ya maendeleo ya jamii. Watumishi 20 wa Wizara watajengewa
uwezo wa ukusanyaji takwimu, ufuatiliaji na tathmini.
Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu
73.
Mheshimiwa
Spika, watumishi ni rasimali muhimu yenye kutekeleza
majukumu ya kila siku ya Wizara. Kutokana na umuhimu wake inahitaji kusimamiwa
vizuri, kujengewa uwezo wa kiutendaji na mazingira mazuri ya kazi ili kuongeza
ufanisi na tija. Katika mwaka 2013/2014, Wizara iliwezesha watumishi 62 kupata
mafunzo ya muda mrefu na mfupi, ndani na nje ya nchi ili kuwaongezea ujuzi na
utaalamu katika utekelezaji wa majukumu yao. Katika mwaka 2014/15, Wizara yangu
itaendelea kuwawezesha watumishi 84 kupata mafunzo mbalimbali ya muda mfupi na mrefu ndani ya
nchi.
74. Mheshimiwa Spika, katika kuwapatia motisha
wafanyakazi, Wizara yangu kwa mwaka 2013/14, ilipandisha vyeo watumishi 126 na
kuwabadilisha kada watumishi wanne. Aidha, watumishi 86 walithibitishwa kazini.
Kwa kipindi cha mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuwapandisha vyeo watumishi
wake kwa mujibu wa Miundo ya Utumishi wa Kada zao na Sera ya Menejimenti na
Ajira katika Utumishi wa Umma ili kuongeza tija katika utendaji kazi.
75. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekuwa
ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi hasa katika Vyuo vya Maendeleo ya
Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Katika kukabiliana na changamoto hii
mwaka 2013/14, Wizara yangu iliajiri jumla ya watumishi 92 kutokana na kibali cha
ajira kilichotolewa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma chenye
Kumbukumbu Namba BC.62/97/014/11 cha tarehe 4 Juni, 2012. Kwa mwaka 2013/14
Wizara iliwasilisha maombi ya kibali cha ajira ya watumishi 603. Katika mwaka
2014/15, Wizara inatarajia kuendelea kuajiri watumishi wengine ili kuendelea
kupunguza pengo lililopo.
76. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya
utendaji kazi kwa watumishi, mwaka 2013/14, Wizara iliwapatia watumishi
vitendea kazi mbalimbali. Kwa mwaka 2014/2015, Wizara yangu itajenga eneo la
kuegesha magari la Makao Makuu ya Wizara, kununua jenereta na kuendelea
kuwapatia wafanyakazi vitendea kazi mbalimbali.
Aidha, Wizara itawawezesha watumishi kushiriki katika mashindano ya SHIMIWI
ili kuboresha afya na kuimarisha mahusiano miongoni mwa watumishi wa Serikali.
77. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara
yangu iliendelea kuwezesha sekta binafsi za ulinzi na usafi kutoa huduma hizo
kwa Wizara kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji kazi na usalama wa
vifaa na mali. Katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuwezesha sekta binafsi
kutoa huduma hizo.
78. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliendeleza
mapambano dhidi ya UKIMWI na Virusi Vya UKIMWI mahala pa kazi. Katika mwaka
2013/14, Wizara iliwapatia watumishi nasaha za namna ya kujikinga na maambukizi
ya Virusi Vya UKIMWI. Katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuhamasisha
watumishi wajitokeze kupima afya zao pamoja na kuwapatia huduma ya viini lishe
na chakula.
Mawasiliano kwa umma
79.
Mheshimiwa Spika, mawasiliano ni nguzo muhimu katika kuwawezesha wananchi kufahamu huduma
zinazotolewa na Wizara na pia kuiwezesha kupata mrejesho kutoka kwa wadau ili
kuboresha huduma hizo. Kwa mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliandaa vipindi vya luninga, radio na
mikutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kuelimisha umma kuhusu masuala ya
maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake, familia, haki za watoto na uratibu wa
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Aidha, Wizara iliandaa matangazo mbalimbali
kupitia magazeti, vipeperushi na mabango.
80.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2013/14, Wizara
pia ilianzisha mawasiliano na umma kupitia mitandao ya kijamii. Mitandao hiyo
ni pamoja na: Blog ya wizara, www.maendeleoyajamiijinsianawatoto.blogspot.com; Facebook ya wizara,
facebook.com/maendeleoyajamii; na twitter ya wizara, Twitter.com/wmjjwtz. Kwa
mwaka 2014/2015, Wizara itaandaa mkakati wa mawasiliano na kuendelea kuwezesha
mawasiliano kwa umma kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii,
radio, luninga, magazeti, gari la sinema, majarida, vipeperushi na uhamasishaji
jamii kwa kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya kata,
wilaya na mkoa.
E: HITIMISHO
81.
Mheshimiwa
Spika, mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Wizara wa
mwaka 2013/14 na Malengo ya mwaka 2014/15 yanaonesha jinsi Wizara yangu ilivyo
na umuhimu katika kuleta usawa wa jinsia, upatikanaji wa haki na ustawi wa
watoto, ongezeko la ajira kwa vijana na ushawishi wa jamii katika kupokea na
kutekeleza miradi ya maendeleo endelevu. Ili Wizara itekeleze vema majukumu
yake inahitaji ushirikiano mkubwa wa wadau mbalimbali na rasilimali fedha za
kutosha.
F: SHUKRANI
82.
Mheshimiwa
Spika, napenda sasa kumshukuru sana Naibu Waziri,
Mheshimiwa Dk. Pindi Hazara Chana (Mb.), kwa ushirikiano, ushauri na usaidizi
mkubwa anaonipa katika kuongoza Wizara hii. Vilevile, napenda kutoa shukrani za
dhati kwa: Katibu Mkuu, Bibi Anna Tayari Maembe, Naibu Katibu Mkuu, Bibi Nuru
H. M. Millao; Wakurugenzi; Wakuu wa Vitengo; Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Wanawake Tanzania - Bibi Magreth Chacha; Wakuu wa Vyuo; na Wafanyakazi wote wa
Wizara yangu wa ngazi zote, kwa jitihada zao katika utekelezaji wa majukumu ya
Wizara, ambayo ni pamoja na kuniwezesha mimi kuwasilisha hotuba hii mbele ya
Bunge lako tukufu.
83.
Mheshimiwa
Spika, kabla sijamaliza hotuba yangu, sina budi
kuwashukuru wadau wote tunaofanya nao kazi na wengine ambao kwa namna moja au
nyingine tunashirikiana. Peke yetu kama Wizara tusingefikia mafanikio
niliyoyataja. Naomba kupitia Bunge lako tukufu, kutoa shukrani zangu za
dhati kwa wafuatao: Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF), Asasi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA); Mfuko wa Fursa Sawa
kwa Wote (EOTF); Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP); Chama cha Wanasheria
Wanawake Tanzania (TAWLA); Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania
(TAMWA); Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (FAWETA);
Medical Women Association of Tanzania (MEWATA); White Ribon; Plan
International; Save the Children; Mashirika mbalimbali yasiyo ya Kiserikali
pamoja na wale wanaofanya kazi kwa maslahi ya jamii kwa namna moja au nyingine.
Napenda pia kuyashukuru Mashirika kutoka nchi rafiki ambayo yameendelea
kutusaidia na kufanya kazi na sisi. Mashirika hayo ni pamoja na: DFID; GPE;
CIDA; KOICA na UK Education. Aidha, nayashukuru Mashirika ya Umoja wa Mataifa
ambayo ni: UNICEF; UNDP; UNFPA na UN WOMEN kwa misaada yao mbalimbali
iliyofanikisha utekelezaji wa majukumu mengi ya Wizara yangu.
G. MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA
MWAKA 2014/15
84.
Mheshimiwa
Spika, ili Wizara yangu iweze kutekeleza majukumu na
malengo yake kwa mwaka 2014/15, sasa naliomba Bunge lako tukufu liidhinishe
matumizi ya shilingi 30,233,474,000.
Kati ya maombi haya:
(a)
Shilingi
21,215,930,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida;
(b)
Shilingi
12,818,434,000 ni kwa ajili ya mishahara;
(c)
Shilingi
8,397,496,000 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo;
(d)
Shilingi
9,017,544,000 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo shilingi
7,000,000,000 ni fedha za ndani na shilingi 2,017,544,000 ni fedha za nje.
85.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.